Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasimamisha kazi Kamishna
Mkuu wa Uhamiaji Bwana Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji
anayeshughulikia Utawala na fedha Bwana Piniel Mgonja ili kupisha
uchunguzi, kufuatia dosari alizozibaini Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mheshimiwa Charles Kitwanga alipotembelea Idara ya Uhamiaji hivi
karibuni.
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amezitaja dosari hizo kuwa ni pamoja
na tuhuma za rushwa, ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji
wa taratibu za manunuzi na utendaji mbovu.
Balozi
Sefue amesema watendaji hao wakuu wa Uhamiaji wamesimamishwa kazi mara
moja hadi hapo uchunguzi utakapokamilika na kwamba endapo watabainika
kutokuwa na makosa Rais ataamua hatma yao.
Katika Hatua nyingine Rais John Pombe Magufuli amemrejesha Bwana Eliakim Chacha Maswi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, baada ya kukamilisha kazi maalum aliyomtuma kuifanya katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kabla
ya kurejeshwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bwana Maswi
aliteuliwa kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli amefanya
mabadiliko hayo kwa lengo la kumtafuta mtu mwenye utaalamu wa kuendeleza
kazi iliyofanywa na Bwana Maswi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
20 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment